Wanaogombea kitalu cha utalii wapashwa
Chini ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Daudi Ntibenda, kamati hiyo juzi ilikutana na wasimamizi wa kitalu hicho kutoka kila kampuni, Diwani wa Kata ya Kitumbeine kilipo kitalu hicho, baadhi ya viongozi wa vijiji vinavyozunguka na vilivyo ndani ya kitalu.
Iliamuru kuwa mikataba iliyopo kati ya wawekezaji na wanakijiji iheshimiwe kwa mujibu wa sheria. Kampuni ya WWS iliingia mkataba na vijiji 26 vinavyozunguka kitalu cha uwindaji cha Ziwa Natron Kaskazini Kusini utakaomalizika Agosti 15, mwaka huu.
Imeamriwa kuondoka katika eneo hilo na kuzua hali ya wasiwasi miongoni mwa wananchi. Hatua hiyo ya mkuu wa mkoa inatokana na maelezo aliyopewa na msimamizi wa kitalu hicho wa WWS, Alfred Mwakivike na Diwani wa Kata ya Kitumbeine, Timotheo Laizer kwamba kampuni hiyo iliingia mkataba wa miaka miwili kuanzia Agosti 15, 2014 na ambao utamalizika Agosti 15, 2016.
Mgogoro kati ya kampuni hizo unatokana na hatua ya Wizara ya Maliasili na Utalii kuamuru WWS waliokuwa wanaendesha shughuli za uwindaji wa kitalii katika kitalu hicho tangu mwaka 1990, waondoke hapo ifikapo Mei 31, mwaka huu.
Amri hiyo ya wizara ambayo imo katika barua ya Mei 9, mwaka huu iliyosainiwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, pamoja na mambo mengine inaitaka WWS kuondoka katika kitalu hicho na kuipisha Green Mille iendeshe shughuli za uwindaji wa kitalii.
Hatua hiyo ilipingwa na WWS na vijiji hivyo 26 wakidai kuwa wana mkataba utakaomalizika Agosti 15, hivyo kuitaka serikali kuingilia kati suala hilo lililoonekana kuwa na viashiria vya kuleta uvunjifu wa amani iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa.
Mwakivike alimweleza mkuu huyo wa mkoa kwamba pamoja na WWS kuwa na mkataba na vijiji hivyo, tayari walishalipa ada ya kitalu hicho kwa msimu wa uwindaji wa 2016/2017, huku wakiwa wamekamilisha maandalizi ya kuanza kwa msimu wa uwindaji wa utalii ulioanza rasmi jana.
Tayari WWS wamepewa na Mahakama Kuu zuio la muda la utekelezaji wa maagizo hayo ya wizara hadi Julai 6, mwaka huu kesi yao ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi kuhusu barua hiyo ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
0 maoni:
Chapisha Maoni